Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya dunia kuipatia Nepal dola Milioni 500 za usaidizi

Benki ya dunia kuipatia Nepal dola Milioni 500 za usaidizi

Benki ya dunia imetangaza kuwa itaipatia Nepal dola Milioni 500 ili kuendelea kusaidia harakati za nchi hiyo kujikwamua baada ya matetemeko makubwa ya ardhi ya mwezi Aprili na Mei mwaka huu,

Matetemeko hayo yalisababisha vifo vya watu wapatao Elfu Tisa na wengine wengi kujeruhiwa huku makazi ya milimani yakisalia magofu.

Taarifa ya benki hiyo imesema fedha hizo zinasubiri idhinisho la bodi tendaji ya taasisi hiyo ambapo dola Milioni 200 ni kwa ajili ya makazi kwenye maeneo ya watu maskini ilhali dola Milioni 100 zitasaidia serikali kuimarisha sekta ya benki.

Kiwango kilichosalia cha dola Milioni 200 kitaelekezwa kwenye miradi ya Benki ya dunia nchini Nepal na harakati nyingine za ujenzi mpya.

Rais wa Benki ya dunia Jim Yong akizungumzia hatua hiyo amesema taasisi yake iko bega kwa began a wananchi wa Nepal na wanashirikiana na wadau wa kimataifa kuhakikisha nchi hiyo inapata rasilimali inayohitaji ili ikwamuke.