Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo thabiti yanahitaji upinzani thabiti bungeni na unaowajibika: Ban

Maendeleo thabiti yanahitaji upinzani thabiti bungeni na unaowajibika: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesifu harakati za Kyrygzstan za kujikwamua kutoka mzozo wa kikabila wa mwaka 2010 na hatimaye kuanza kujenga taifa lenye ustawi licha ya changamoto za sasa za kuimarisha bunge lake.

Amesema hayo alipohutubia mkutano wa uendelezaji mabunge uliofanyika mji mkuu wa nchi hiyo, Bishkek,  akisisitiza umuhimu wa kuongeza idadi ya wanawake wabunge, sanjari na kutaja kile kinachowezesha bunge kuwa makini…

(Sauti ya Ban)

“Kuhudumia kwa dhati wananchi, bunge linahitaji upinzani ulio machachari, ambao unahoji serikali lakini pia ukiwa na hisia ya uwajibikaji. Mnavyojitahiki kuimarisha demokrasia, nawasihi mkumbuke kuwa kutofautisha mamlaka ya mihimili mikuu mitatu ya dola, unasalia katika kuweka mizania na kuheshimu mamlaka ya kila mhimili, ambayo ni mahakama, serikali na bunge.”

Amesema iwapo mahakama inakuwa mtumwa wa serikali, mfumo wa utendaji hautakuwa thabiti, halikadhalika bunge likianza kufanya kazi za serikali, serikali itaparaganyika.

Ban amesema mafanikio ya Kyrgyzstan yatakuwa na maana zaidi iwapo baadaye mwaka huu itafanya uchaguzi kama ilivyopangwa kwa kuzingatia chaguzi huru na haki zinazotoa fursa kwa kila mwananchi mwenye haki ya kupiga kura kushiriki bila vikwazo vyovyote.