Skip to main content

Raia wa Ukraine bado wakumbwa na ukiukwaji wa haki: Zeid

Raia wa Ukraine bado wakumbwa na ukiukwaji wa haki: Zeid

Licha ya makubaliano ya Minsk ya tarehe 12, Februari mwaka huu yaliyopunguza mapigano, bado raia wa Ukraine wanaendelea kuteseka na kuuawa na makombora, amesema leo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein.

Kamishna Zeid amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya kumi ya ufuatiliaji wa haki za binadamu nchini Ukraine, unaochunguza kipindi cha kati ya Februari 16 hadi Mei 15 mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti hii, bado raia milioni tano wanaoishi kwenye maeneo ya mzozo wanaendelea kukumbwa na kurushwa kwa makombora, mauaji, mateso, biashara haramu ya binadamu na ukiukwaji mbali mbali wa haki zao, huku watu zaidi ya 6,000 wakiwa wameuawa wakati wa kipindi cha ripoti.

Aidha askari na silaha vinadaiwa kutumwa kutoka Urusi, kwa mujibu wa ripoti hii.

Kamishna Zeid amesikitishwa pia na ukosefu wa huduma za msingi na upatikanaji wa sheria.

Hatimaye amesema kuwa mamilioni ya wanawake, wanaume na watoto wa kawaida nchini Ukraine wameathirika na hali ngumu na ghasia, wakiishi kwenye hali ya woga kwa zaidi ya mwaka moja sasa, wengi wao wakiwa wamepoteza makazi na riziki zao bila dalili yeyote ya haki, uwajibikaji au fidia.”