Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yapata wasiwasi juu ya hali ya kibinadamu Burundi

WFP yapata wasiwasi juu ya hali ya kibinadamu Burundi

Shirika la Umoja wa MAtaifa la Mpango wa Chakula WFP limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kibinadamu nchini Burundi, likisema mzozo wa kisiasa unaweza kusababisha tatizo la uhakika wa chakula nchini humo, tayari Burundi ikikumbwa na tatizo hilo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Geneva, Elisabeth Byrs, msemaji wa WFP, amesema tayari wanasambaza vyakula kwa wakimbizi 60,000 nchini Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Tanzania.

Ameongeza kwamba WFP iko tayari kusaidia watu walioathirikla na mzozo ndani ya nchi, shirika hilo likiwa limebaini watu 500 ambao ni wakimbizi wa ndani.

(Sauti ya Byrs)

"Kabla ya mzozo, watu milioni 1.1 nchini humo walikuwa wanakumbwa na ukosefu wa uhakika wa chakula. Asilimia 58 ya watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano walikuwa wameathirika na utapiamlo, kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango vya juu kabisa duniani."

Kabla ya mzozo, WFP ilikuwa inasaidia zaidi ya watu milioni moja nchini Burundi kupitia usaidizi wa vyakula, kilimo na mlo wa shuleni.

Bi Byrs ameeleza pia kuwa WFP imekusanya fedha za dharura kwa ajili ya operesheni hizo lakini ufadhili bado unahitajika ili kuendelea kusambaza msaada..