Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Burundi, watoto watano wauawa: UNICEF yataka walindwe

Mzozo Burundi, watoto watano wauawa: UNICEF yataka walindwe

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetaka mamlaka nchini Burundi na pande zote kwenye mzozo unaoendelea kuhakikisha watoto hawahusishwi kwenye vurugu hizo ikiwemo maandamano.

UNICEF imesema hayo wakati huu ambapo tangu kuanza kwa mzozo imeripotiwa vifo vya watoto watano ikiwemo kifo kimoja hapo Alhamisi kwenye mji mkuu Bujumbura hivyo msemaji wake Christopher Boulierac anasema..

(Sauti ya Boulierac)

“Watoto popote pale wana haki ya usalama na kulindwa dhidi ya ghasia. Watoto na vijana nchini Burundi hawapaswi kushiriki kwenye maandamano ya kisiasa au vitendo vyovyote vitakvyohatarisha usalama wao au hawapaswi kuhamasishwa kushiriki kwenye mazingira yoyote ya chuki.

UNICEF imesema hivi sasa inashirikiana na ofisi ya haki za binadamu kubaini watoto ambao pengine walikamatwa kinyume cha sheria na kuwekwa korokoroni mjini Bujumbura ili hatimaye waachiliwe huru na waungane na familia zao.

Maandamano yalianza nchini Burundi tarehe 26 mwezi uliopita baada ya Rais Pierre Nkurunzishwa kupitishwa kuwania nafasi ya urais kwa awamu ya tatu.