Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio lapitishwa UM kulinda maeneo ya urithi wa kitamaduni Iraq

Azimio lapitishwa UM kulinda maeneo ya urithi wa kitamaduni Iraq

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo kwa kauli moja limepitisha azimio lenye lengo la kuokoa amali za urithi wa dunia nchini Iraq ambazo zimekuwa zikishambuliwa na kuharibiwa na magaidi wa kikundi cha ISIS au Da’esh.

Azimio hilo mathalani linasisitiza umuhimu wa dhima ya Umoja wa Mataifa katika kuimarisha uwezo wa nchi wanachama kulinda urithi huo wa kibinadamu wakati huu ambapo maeneo ya kihistoria nchini Iraq yameharibiwa na mengine kutokomezwa kabisa na magaidi hao.

Akizungumza baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, mwakilishi wa kudumu wa Iraq kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mohammed Ali al-Hakim amekaribisha hatua hiyo akisema ni muhimu siyo tu kwa binadamu wote duniani lakini zaidi kwa Iraq kwa kuwa ..

(Sauti ya Balozi al-Hakim)

"Uharibifu wa urithi wa utamaduni wa Iraq ambao ni kitovu cha ustaarabu ni jambo la hatari kama ilivyo mauaji ya kikatili wanayofanyiwa wananchi wa Iraq na kwamba lengo ni kufuta historia ya ustaarabu wa Iraq na wingi wa tamaduni za nchhi hii ambazo zimekusanywa vizazi na vizazi.”

 Amesema azimio la leo linaimarisha jitihada za Iraq za kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kushirikiana na Umoja wa Mataifa na wadau katika kudhibiti usafirishaji haramu na biashara ya magendo ya turadhi hizo kunakotumiwa kufadhili vitendo vya kigaidi.