Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Klabu ya soka ya Valencia yapigia chepuo usawa wa jinsia

Klabu ya soka ya Valencia yapigia chepuo usawa wa jinsia

Harakati za Umoja wa Mataifa za kupigia chepuo usawa wa kijinsia umeingia hatua mpya baada ya Shirika lake linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women kuingia ubia na klabu ya soka ya Hispania Valencia.

Ubia huo wa aina yake umetiwa saini jijini New York na kushuhudiwa na wasakata kabumbu wa klabu hiyo ya kulipwa ambapo nembo ya UN-women itachapishwa katika jezi za wanasoka hao watakazotumia wakati wa mashindano ya Ulaya kama vile kombe la mabingwa barani humo.

Akizindua ubia huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema wamejizatiti kuwajumuisha wanaume na wavulana kwenye kuchagiza usawa wa jinsia kupitaa kampeni ya #HEforSHe.

Amesema wachezaji wa Valencia ni mfano thabiti wa kuigwa na wataonyesha kwa vitendo mashabiki wao siyo tu Ulaya bali duniani kote kupitia kandanda.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa klabu hiyo ya soka ya Valencia, Lay Hoon Chan ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika historia ya miaka 96 ya klabu hiyo amesema ni heshima kubwa kwao kushirikiana na UN Women kuhamasisha jambo hilo adhimu.

Miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Valencia walioshiriki tukio hilo ni Dani Parejo, Shkodran Mustafi, Paco Alcacer na Alvaro Negredo.