Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wenye njaa duniani sasa ni chini ya 800

Wenye njaa duniani sasa ni chini ya 800

Idadi ya watu wenye njaa duniani sasa imeshuka hadi milioni 795, ikiwa imepungua kwa milioni 216 ikilinganishwa na ilivyokuwa kati ya mwaka elfu moja kenda mia tisini na kenda mia tisini na mbili, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu njaa.

Ripoti hiyo ya hali ya usalama wa chakula duniani kwa mwaka 2015, imechapishwa na Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD na Shirika la Mpango wa chakula, WFP.

Ripoti inasema kuwa kuenea kwa lishe duni, ambacho ni kipimo cha idadi ya watu wasioweza kupata chakula cha kutosha ili kuwa na maisha yenye afya, kumepungua katika maeneo yanayoendelea hadi asilimia 12.9 ya idadi ya watu, ikiwa imeshuka kutoka asilimia 23.3 miaka ishirini na mitano iliyopita.

Nchi 72 kati ya 129 zilizofuatiliwa na FAO zimetimiza lengo la milenia la kupunguza kuenea kwa lishe duni kwa nusu ifikapo mwaka 2015, huku maeneo yanayoendelea yakishindwa kutimiza lengo hilo kwa kiwango kidogo mno.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa matukio ya majanga ya hali ya anga, majanga ya kiasili, misukosuko ya kisiasa na mizozo imezuia kupiga hatua katika baadhi ya nchi, zikiwemo nchi 24 za Afrika ambazo sasa zinakumbwa na tatizo la njaa. Pietro Gennari, ni Mkurugenzi wa Idara ya Takwimu katika FAO

"Tuna kundi la nchi ambazo tumetambua  kuwa zimekuwa katika migogoro ya muda mrefu, ambazo hali zao zinafanana: nchi ambazo zimepigwa na matatizo, zina kiwango cha chini cha uhimili na kiwango cha juu cha kutokuwa na usalama wa chakula. Matatizo haya ya nje ama ni maafa ya asili au maafa yaletwayo na mwanadamu. Nchi hizi kwa ujumla zimekuwa na mafanikio madogo sana katika kupunguza njaa. Nchi pekee miongoni mwa nchi hizi zenye matatizo ya muda mrefu ambayo imeweza  kufikia lengo la MDG’s  ni Ethiopia"