Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya amani ya Yemen yaahirishwe, serikali haiko tayari: Ban

Mazungumzo ya amani ya Yemen yaahirishwe, serikali haiko tayari: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemwomba Mjumbe wake maalum kwa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, kuahirisha mazungumzo ya amani kuhusu nchi hiyo yaliyotarajiwa kuanza huko Geneva, Uswisi tarehe 28, mwezi huu wa Mei.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Ban amesema uamuzi huo unafuatia ombi la serikali ya Yemen na wadau wengine kutaka muda zaidi wa kujiandaa huku akisema atajitahidi kuitisha mkutano haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo Katibu Mkuu amenukuliwa akisema amesikitishwa sana kuwa haikuwezekana kufanya mkutano huo muhimu mapema, na amekariri wito wake kwa pande zote wa kushiriki kwenye mazungumzo hayo kwa nia njema akisisitiza kuwa suluhu ya mzozo wa Yemen ni makubaliano jumuishi ya kisiasa.

Akimulika hali ya kibinadamu nchini humo, Katibu Mkuu amezisihi pande zote kujali mateso ya raia wa Yemen na kushirikiana na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika utaratibu wa amani.