Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikao cha 68 cha baraza kuu la afya duniani kimeanza Geneva:WHO

Kikao cha 68 cha baraza kuu la afya duniani kimeanza Geneva:WHO

Kikao cha 68 cha baraza kuu la afya duniani mwaka 2015 kimeanza mjini Geneva Uswisi. Akizungumza katika ufunguizi wa kikao cho mkurugenzi mkuu wa WHO Bi Margareth Chan amesema vitisho vya afya vimeongezeka maradufu sambamba na juhudi za uwezo wa kukabiliana navyo.

Amesema dunia inapaswa kuwa tayari wakati wote hasa kupambana na majanga makubwa ya milipuko ya magonjwa akitolea mfano ugonjwa wa ebola ambao amesema umelitikisa shirika la afya. Amesisitiza kwamba hakuna mradi wowote wa afya utakaoweza kufanikiwa kwa muda mrefu kama hakutakuwa na mifumo bora ya afya inayofanya kazi.

(SAUTI YA MARGARET CHAN)

"Mlipuko wa Ebola umetikisa msingi wa shirika hili . Kama ilivyoelezwa katika tathmini ya ripoti ya mpito, mlipuko huu uliweka bayana kazi ya WHO na ni wakati wa kihistoria kisiasa kwa viongozi wa dunia kuipa WHO umuhimu mpya na kuiwezesha kuongoza katika afya kimataifa. Nawasihi nyote kuhakikisha inawezekana na kwa upande wangu nitafanya kila niwezalo."

Kikao hicho cha kila mwaka ambacho kitaendelea hadi Mai 26, huwaleta pamoja wawakilishi kutoka nchi zote wanachama wa WHO.