Skip to main content

Ban aomba nchi zichangie zaidi kukwamua Nepal

Ban aomba nchi zichangie zaidi kukwamua Nepal

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kufanya juhudi zaidi, ili kufikisha misaada kwa watu wenye mahitaji makubwa nchini Nepal, takriban wiki tatu tangu tetemeko la kwanza la ardhi kulikumba taifa hilo. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte

(Taarifa ya Priscilla)

Katibu Mkuu amesema hayo mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo limekutana kujadili kuhusu uimarishaji wa uratibu na usaidizi wa kibinadamu nchini Napal, aki sisitiza umuhimu wa kufikisha misaada kwa kila mtu mwenye mahitaji wiki chache zijazo.

Ban amesema usaidizi pia unahitajika haraka kufungua nafasi za ajira kwa dharura, kuwezesha ukwamuaji wa uchumi na kuinua vitega uchumi.

“Misaada ya dharura pekee haitoshi. Kunusuru maisha ya watu ni muhimu, lakini watu ni lazima pia waweze kuendeleza maisha yao. Wanataka kuwa na mustakhbali. Nepal imesambaratishwa. Miaka mingi ya hatua za maendeleo imefutwa.

Ban amesema kuwa amefurahishwa na kutiwa moyo na mshikamano ulioonyeshwa na nchi wanachama kwa Nepal wakati huu mgumu.

“Nashukuru juhudi za Baraza Kuu kuwasaidia watu wa Nepal wakabiliane na hasara kubwa waliyoipata. Nashukuru nchi zilizochangia kufikia sasa. Lakini bila usaidizi zaidi na mathubuti, watu zaidi watapoteza uhai.

Kufikia sasa, ombi la ufadhili kwa Nepal limepokea asilimia 14 tu ya mchango wa fedha, likiwa na pengo la dola milioni 365. Baadaye Baraza Kuu limepitisha azimio la kuunga mkono wito wa kuisadia Nepal.