Skip to main content

Kongamano lafanyika Nairobi kuchagiza ukuaji unaojali mazingira

Kongamano lafanyika Nairobi kuchagiza ukuaji unaojali mazingira

Jukwaa la kwanza kuhusu ukuaji unaojali mazingira kwa ukanda wa Afrika, limefunguliwa leo mjini Nairobi, likihudhuriwa na rais Uhuru Kenyatta na wajumbe zaidi ya 200, wakiwemo mawaziri wa mazingira kutoka nchi za Afrika, watunga sera, na wataalam wa kimataifa wa uchumi na mazingira.

Kongamano hilo la siku mbili linalenga kutambua vizuizi kwa maendeleo endelevu barani Afrika, na njia za kuvigeuza vizuizi hivyo kuwa fursa  za ukuaji unaojali mazingira na kuboresha hali ya maisha, na litaangazia njia mpya za ufadhili kwa ukuaji unaojali mazingira, ukuaji endelevu wa miji na mifumo endelevu ya maisha.

Jukwaa hilo pia linatarajiwa kuchagiza mazungumzo kuhusu uzalishaji wa nishati endelevu na inayotegemewa, ukuaji endelevu wa viwanda na kuongeza teknolojia ya kisasa kwenye bara la Afrika.

Jukwaa hilo limeandaliwa kwa pamoja na serikali ya Kenya, serikali ya Denmark na Shirika la Mpango wa Mazingira, UNEP, chini ya jukwaa la kimataifa la ukuaji wenye kujali mazingira, 3GF, ambalo hupatanisha wadau kuhusu ukuaji jumuishi na unaojali mazingira.