FAO yatoa muongozo wa kuwalinda watoto dhidi ya kemikali na dawa za sumu
Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la Kilimo na Chakula(FAO) na lile la Kazi Duniani(ILO) yametoa muongozo wa kuwalinda watoto dhidi ya dawa za sumu wanazozipata kwa kujihusisha katika ajira katika umri mdogo.
Kwa mujibu wa ILO takribani watoto milioni 100 kote duniani wasichana na wavulana walio katika umri kati ya miaka mitano na 17 wanajihusisha na ajira za utotoni katika kilimo ambapo wengi wao hutoa kemikali zenye sumu wakiwa katika kazi za mashambani.
FAO inasema katika taarifa yake kuwa kupitia mafunzo iliyoendesha kwa kushirikiana na ILO, yaliyotoa muongozo , wafanyakazi wa ugani barani Afrika na sehemu nyiginezo wanajishughulisha katika kutokomeza madawa ya sumu mashambani kwa kushirikiana na jamii za vijijini.
FAO imesema kuwa watoto wanaweza kuathirika zaidi kwa sumu kuliko watu wazima na pia wanaweza kupata madhara ya muda mrefu ya afya na ustawi wao.