Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yapongeza ajenda iliyopendekezwa na EU kuhusu uhamiaji

UNHCR yapongeza ajenda iliyopendekezwa na EU kuhusu uhamiaji

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR limeyapongeza mapendekezo ya kamisheni ya Muungano wa nchi za Ulaya, EU, ambayo yametangazwa leo kwa ajili ya kukabiliana na maelfu ya wakimbizi na wahamiaji wanaowasili Ulaya kupitia Bahari ya Mediterenia.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kuimarisha njia za kunusuru maisha ya wahamiaji baharini na kuboreshwa njia za kuruhusu watu wanaokimbia vita kuingia Ulaya kwa njia halali, pamoja na kuwezesha kugawanya vyema zaidi wakimbizi hao miongoni mwa nchi za EU.

Mapendekezo hayo pia yanajumuisha mbinu za kukabiliana na baadhi ya sababu zinazochangia kuwalazimu watu kujikuta katika mikono ya walanguzi, zikiwemo hali mbaya za maisha wanazokumbana nazo wakimbizi hao katika nchi wanakokimbilia kwaza kutafuta hifadhi na wanakopitia.

Msaidizi wa Kamishna Mkuu wa UNHCR kuhusu ulinzi wa Wakimbizi, Volker Türk, amesema mapendekezo hayo yanawakilisha ufanisi mkubwa katika udhibiti wa usafiri wa wakimbizi na uhamiaji. Ameongeza kuwa sasa ni muhimu kwamba mapendekezo hayo yazingatiwe haraka na kutekelezwa kikamilifu kwa ajili ya kuokoa maisha.