Skip to main content

Ofisi ya haki za binadamu yaomba uchunguzi ufanyike Yemen

Ofisi ya haki za binadamu yaomba uchunguzi ufanyike Yemen

Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu Ravina Shamdasani amesema tayari raia 646 wamefariki dunia kutokana na mashambulizi yanayoendelea nchini Yemen tangu Machi tarehe 26 mwaka huu, na wengine 1,364 wamejeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi msemaji huyo ameongeza kwamba nyumba nyingi za raia zimeharibiwa na makombora. Ametaja mfano wa shambulio lililotokea Mei mosi ambapo raia 27 waliuawa na kombora lililokuwa linadaiwa kulenga nyumba ya kiongozi wa Houthi, kwenye eneo la Sana’a.

Aidha amesema kwamba ukiukwaji wote wa haki za binadamu na haki ya kibinadamau ya kimataifa unaotokea wakati wa mashambulizi hayo utapaswa kuchunguzwa, akikariri kwamba raia ambao hawashiriki kwenye mapigano hawapaswi kulengwa.

Hatimaye Bi Shamdasani amezingatia hali ya watu wenye ulemavu, akieleza kwamba watu milioni tatu wanaoishi na ulemavu wanazidi kukabiliana na changamoto katika maisha yao ya kila siku.