Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbivu na mbichi Liberia kuhusu Ebola kufahamika Mei 9:UNMIL

Mbivu na mbichi Liberia kuhusu Ebola kufahamika Mei 9:UNMIL

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia, Karen Landgren amewaeleza wajumbe wa Baraza la usalama kuwa wakazi wa taifa hilo la Afrika Magharibi wanasubiri kwa hamu kufahamu iwapo wamefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa Ebola.

Akihutubia Baraza hilo wakati wa kikao kuhusu hali ilivyo nchini Liberia, Bi. Landgren ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Liberia, UNMIL ukweli wa mambo kuhusu hali ya ebola utafahamika tarehe Tisa mwezi huu.

(Sauti ya Landgren)

“Iwapo hakuna kisa kipya kitakuwa kimethibitishwa hadi siku hiyo, shirika la afya ulimwenguni litatangaza rasmi kutokomezwa kwa Ebola Liberia. Baada ya takribani miezi 14 ya zahma ya Ebola, hizi zitakuwa ni habari njema kwa wananchi wa Liberia.”

Amesema tayari ujumbe wa umoja wa mataifa wa kushughulikia dharura ya Ebola, UNMEER tayari umefunga ofisi yake huko Liberia na kukabidhi majukumu yake kwa UNMIL na mashirika ya Umoja wa Mataifa na sasa kilichobakia ni wananchi kuwa makini.

Kuhusu kipindi cha mpito cha UNMIL kukabidhi majukumu yake kwa serikali, Bi. Landgren amesema harakati zinaendelea salama na kwamba kuna kundi maalum la pamoja linalofuatilia mpango huo lakini changamoto ni ufadhili wa fedha katika mipango ya kuimarisha usalama.