Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya mwaka mmoja, Ban aendelea kuomba wasichana wa Chibok waachiliwe huru

Baada ya mwaka mmoja, Ban aendelea kuomba wasichana wa Chibok waachiliwe huru

Leo ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kutekwa nyara kwa wasichana 276 kwenye shule yao ya Chibok, kaskazini mashariki mwa Nigeria, na kundi la Boko Haram, jamii ya kimataifa haipaswi kusahau wasichana ambao bado hawajaachiliwa huru, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Katika taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake, Bwana Ban amenukuliwa akisema kwamba hataacha kuomba waachiliwe huru na warudishwe salama kwa familia zao.

Aidha Katibu Mkuu ameeleza kuwa kundi la waasi wa Boko Haram limezidi kutekeleza mashambulizi dhidi ya wasichana na wavulana wa Nigeria na nchi jirani kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, akilaani vitendo vyote vya uhalifu vinavyofanywa na Boko Haram, ikiwemo kutumia wasichana kujitoa muhanga, na kushambulia shule mara kwa mara.

Ban Ki-moon amekariri uungwaji mkono wake na serikali pamoja na raia wa ukanda huo katika jitihada zao za kupambana na Boko Haram, akisisitiza kwamba mapigano hayo yanapaswa kufanyika kwa kuheshimu sheria za kimataifa.