Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kasi ndogo ya kiwango cha biashara duniani kuendelea 2015/2016

Kasi ndogo ya kiwango cha biashara duniani kuendelea 2015/2016

Shirika la biashara duniani WTO limesema kuna matarajio ya kukua japo kwa kiwango kidogo cha biashara duniani ifikapo mwakani.

Mkurugenzi Mkuu wa WTO Robert Azevêdo amesema hayo kufuatia ripoti ya wachumi wa shirika hilo iliyotolewa Jumanne inayosema kuwa kiwango hicho kiliongezeka kutoka asilimia 2.8 mwaka 2014 hadi asilimia 3.3 mwaka huu huu huku mwakani ikitarajiwa kufikia asilimia 4.0.

Bwana Azevêdo ametaja mambo yanayoweza kukwamisha kufikiwa kwa viwango hivyo..

(Sauti ya Azevêdo)

“Kiwango kidogo cha ukuaji wa pato la ndani, GDP kuliko ilivyotarajiwa. Kwa hiyo kama nilivyosema iwapo GDP inakuwa asilimia Tatu au juu kidogo tu ya asilimia tatu, kiwango cha ukuaji wa biashara nacho kitaporomoka hasa iwapo kiwango cha ukuaji katika nchi zinazoibuka kiuchumi hakitaimarika. Jambo lingine ni kuendelea kupanuka kwa mivutano ya kisiasa baina ya nchi. Lingine ni uwezekano wa sera tata za kifedha kutoka nchi tajiri ambazo zinaweza kuchochea kabisa na kubadili mwelekeo wa viwango vya ubadilishaji wa fedha na mwelekeo wa mitaji ambayo pia vitaathiri mazingira ya biashara.”

Halikadhalika Mkurugenzi Mkuu huyo wa WTO amependekeza kuondoa vikwazo vya biashara, kuongeza wigo na uwezo wa nchi kupeleka bidhaa zao kwenye nchi zingine pamoja na kuondoa sera zinazokwamisha ushindani.

WTO inasema kiwango kiwango cha ukuaji wa biashara kitabakia chini ya wastani wa asilimia 5.1 na ni cha chini kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1990.