Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu inadorora kwa kila saa, Yemen

Hali ya kibinadamu inadorora kwa kila saa, Yemen

Hali ya kibinadamu nchini Yemen inaendelea kuzorota kila uchao amesema Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini humo Johannes Van der Klaauw wakati huu ambapo mzozo huo unaathiri  majimbo 15 kati ya 22 na mamilioni ya watu wakiwa hatarini kujeruhiwa au kupoteza maisha kwa sababu ya vita.

Vita hivyo vimeshuhudia  mashambulizi ya angani huku huduma muhimu kama vile afya, maji safi na salama na chakula zikidorora.

Umoja wa Mataifa unasema kabla yz kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini humo, watu milioni 16 walikuwa wanahitaji misaada ya kibinadamu  kwa ajili ya mahitaji muhimu kama anavyofafanua van der Klaauw.

(sauti ya Johannes)

“Mzozo umesababisha kuongezeka kwa mahitaji  ya makundi yaliyo hatarini huku wengine wakitumbukia kwenye hatari kubwa. Wananchi wa Yemen  wanateseka kupata  huduma za afya, maji, chakula na mafuta- mahitaji ambayo ni muhimu kwa kuishi.”

Maelfu ya watu wa Yemen wamekimbia makwao kuelekea nchini Djibouti na Somalia kwa boti.

Tangu tarehe 19 mwezi uliopita,  takriban watu 640 wamefariki dunia  huku zaidi ya 2200 wakipata majeraha kutokana na mashambulio ya anga yanayofanywa na nchi za ukanda huo zikiongozwa na Saudi Arabia.