Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la waajiriwa wenye umri zaidi ya miaka 55 ni changamoto kwa waajiri: ILO

Ongezeko la waajiriwa wenye umri zaidi ya miaka 55 ni changamoto kwa waajiri: ILO

Shirika la kazi duniani ILO limesema idadi ya waajiriwa wenye utu uzima duniani imeongezeka na kufikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudia duniani na hivyo kuleta changamoto kwenye sekta ya utendaji kazi.

ILO katika chapisho lake jipya kuhusu Ajira dunian na mtazamo wa kijamii, imesema hali hiyo inasababisha mabadiliko ya mahitaji sehemu za kazi.

Mathalani imesema kiwango cha wafanyakazi wenye umri wa miaka 55 na kuendelea kimeongezeka kutoka asilimia 10.5 mwaka 1990 hadi asilimia 14.3 mwaka 2014, kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Mchumi mwandamizi wa ILO Ekkehard Ernst anasema kadri wafanyakazi wanapozeeka uchumi nao unaongezeka, lakini kuna changamoto.

(Sauti ya Ernst)

"Ni kwamba, sekta za kiuchumi zenye wafanyakazi walio na umri we umri wa utu uzima kwa wastani zinaweza kushuhudia ongezeko la kasi ya uchumi. Wafanyakazi hao  wanaonekana kuwa kichocheo cha ukuaji uchumi kutokana na uzoefu wao mkubwa unaoweza kusaidia kubaini mathalani iwapo teknolojia mpya itakuwa na manufaa kwenye mchakato mzima wa kazi. Lakini pindi kasi ya uzee inapoongezeka kunakuwepo na pengo la stadi walizonazo na zinazotakiwa na hiyo inaweza kuwa ni gharama kwa kuwa kampuni zinahitaji kuhakikisha sehemu za kazi zinakidhi mahitaji ya wafanyakazi wazee.”

Ili kushughulikia changamoto hiyo ILO inasema wafanyakazi wazee washawishiwe kubakia kwenye ajira, halikadhalika kuajiri zaidi wanawake.