Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Masjala ya aina yake yazinduliwa kuimarisha juhudi za usaidizi duniani

Masjala ya aina yake yazinduliwa kuimarisha juhudi za usaidizi duniani

Shirika la afya duniani, WHO limezindua masjala itakayoorodhesha wataalamu  wa afya na mashirika ya usaidizi kwa lengo la kuchukua hatua haraka pindi milipuko ya kiafya inapotokea.

Uzinduzi huo umefanyika leo huko Geneva, Uswisi  ambapo kupitia masjala hiyo, serikali zilizokumbwa na majanga au dharura zinaweza kupata kiwango cha hali ya juu cha msaada kutoka majopo ya wataalamu wa afya wa kigeni yaliyosajiliwa.

WHO inasema imechukua hatua hiyo ili kuepusha changamoto zinazotokea pindi watoa huduma wa kujitolea wanapofika kwenye nchi zenye majanga ambapo uratibu wa juhudi zao za usaidizi wao hukumbwa na matatizo ikitolea mfano tetemeko la ardhi la Haiti mwaka 2010

Chini ya mfumo huo mpya ni wataalamu au mashirika yaliyosajiliwa tu kwenye mfumo huo ndiyo yatakayoruhusiwa kwenda kwenye maeneo yenye dharura kutoa msaada.

Dkt. Ian Norton ni mmoja wa wahusika walioandaa mradi huo.

Masjala hiyo inasaka kutoa hakikisho la mchakato wa uhakika na unaotambulika wa kutoa usaidizi thabiti na salama pindi jamii zinapokumbwa na tsunami, vimbunga, mafuriko, Ebola au kipindupindu au mlipuko wowote ule unaoweza kutokea. Si sahihi kwa daktari au muuguzi kurukia tu kwenye ndege na begi lake tayari kwenda kushughulikia udharura.”

Katika mwaka wa kwanza wa mradi huo WHO inatarajia mashirika 150 ya misaada kujiorodhesha, na timu zipatazo 400 kujumuisha majina yao katika miaka ijayo.