Skip to main content

Tanzania, Kenya na Msumbiji zatajwa ripoti ya WMO 2014

Tanzania, Kenya na Msumbiji zatajwa ripoti ya WMO 2014

Leo ikiwa ni siku ya utabiri wa hali ya hewa, Shirika la Kimataifa la utabiri wa hali ya hewa WMO limesema mwaka 2014 ulikuwa na joto kali zaidi kihistoria, maeneo mengi ya dunia yakiwa yamekumbwa pia na mafuriko. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Katika ripoti yake iliyotolewa leo, WMO imesema kiwango cha halijoto kilizidi kwa nusu nyuzi joto kwa kipimo cha Selsiyasi kwa wastani wa kiwango hicho. Aidha mafuriko makali yameathiri nchi mbali mbali katika kila bara la dunia, zikitajwa nchi za Kenya, Somalia, Msumbiji na Tanzania.

Halikadhalika, WMO imemulika ujuzi wa utabiri wa hali ya hewa, ambao imesema umesaidia kuokoa maelfu ya maisha duniani kote, kupitia mifumo bora ya kupima hali ya hewa na kutoa tahadhari dhidi ya majanga.

Katika ujumbe wale kwa siku ya utabiri wa hali ya hewa , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema matukio kama vile ukame, dhoruba au mafuriko yamesababisha vifo vingi na hasara kubwa za kiuchumi.

Akiongeza kwamba mabadiliko ya tabianchi yanaathiri usalama wa chakula na upatikanaji wa maji katika maeneo mengi ya dunia, Ban amesisitiza umuhimu wa utabiri bora wa hali ya hewa ili kuwezesha viongozi kuchukua maamuzi.