Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushiriki wa wanawake kwenye vyama vya ushirika umeongezeka:Utafiri

Ushiriki wa wanawake kwenye vyama vya ushirika umeongezeka:Utafiri

Ushiriki wa wanawake kwenye vyama vya ushirika umeongezeka miongo miwili iliyopita na hivyo kuleta mabadiliko katika maisha yao.

Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti wa pamoja uliofanywa kwa njia ya mtandao na shirika la kazi duniani, ILO na shirikisho la vyama vya ushirika duniani, ICA.

Rais wa ICA Dame Pauline Green wa ICA amesema utafiti huo umeonyesha kuwa ushiriki huo umepunguza umaskini miongoni mwa wanawake wanaoshiriki kwenye vyama hivyo na kutaja kuwa ni moja ya njia ya kuwezesha wanawake kuishi maisha yenye utu na kuepukana na ghasia na ukatili.

Naye Mkuu wa vyama vya ushirika kwenye ILO Simel Esim amesema vyama vya ushirika vina historia ya kuchangia usawa na uwezeshaji wa kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo taasisi hizo mbili zimetaka serikali kuweka mazingira bora zaidi kwa vyama hivyo vya ushirika ili viweze kuboresha zaidi mchango wao kwa wanawake.

Utafiti ulihusisha watu 600 kutoka vyama vya ushirika, mashirika yasiyo ya kiraia, wasomi na wafanyakazi wa umma kutoka maeneo mbali mbali duniani.