Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baghdad yaathirika zaidi mzozo wa Iraq: UNAMI

Baghdad yaathirika zaidi mzozo wa Iraq: UNAMI

Zaidi ya wau 1,100 wameuawa nchini Iraq mwezi uliopita wa Februari ilhali wengine zaidi ya 2,200 wamejeruhiwa, na hiyo ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na ofisi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNAMI.

Taarifa ya UNAMI inasema idadi hiyo inajumuisha raia na askari na kwamba eneo lililokuwa na wahanga wengi zaidi ni mji mkuu  Baghdad ukifuatia na Diyala.

Hata hivyo UNAMI imeonya kuwa imekumbwa na wakati mgumu kuthibitisha kiwango cha waliouawa na majeruhi kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo jimbo la Anbar.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq ambaye pia ni mkuu wa UNAMI, Nickolay Mladenov amesema mashambulio ya kila siku yanayofanywa na magaidi wa ISIL au Da’esh yanalenga wairaq wote.

Amesema wanatiwa hofu Zaidi kutokana na ripoti za vitendo vya visasi vinavyofanywa na vikundi vilivyojihami kwenye maeneo ambayo hivi karibuni yalikombolewa kutoka ISIL.

Amesisitiza kuwa suluhu la kijeshi pekee dhidi ya ISIL haiwezi kuleta matunda na hivyo anaunga mkono wito wa mara kwa mara wa umoja unaotolewa na Waziri Mkuu wa Iraq na spika wa bunge.

Bwana Mladenov amesema juhudi zozote za kufanikisha umoja kupitia maridhiano ni lazima zizingatia katiba na ushiriki wa kina wa viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii nchini Iraq.