Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umuhimu wa radio kwa watoto na wanawake

Umuhimu wa radio kwa watoto na wanawake

Tarehe 13 mwezi Februari ni siku ya redio duniani, ambapo mwaka huu inafanyika wakati matangazo ya Redio ya Umoja wa Mataifa yakitimiza miaka 69. Katika ujumbe wake kwa mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni, UNESCO, likitoa wito wa kushirikisha zaidi vijana katika vyombo vya habari.Mkurugenzi mtendaji wa UNESCO Irina Bokova amesema mara nyingi vijana wa kike na wa kiume wenye umri wa chini ya miaka 30 wanatengwa katika kuandaa na kutangaza vipindi vya radio, na kwa mantiki hiyo, amevisihi vyombo vya habari na hasa redio kuwapa vijana nafasi ya kujieleza.

Nchini Tanzania hilo limeanza kutendeka  na mtandao wa wanahabari watoto, ambao, kupitia usaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto, UNICEF , unahamasisha watoto kujifunza utalaam wa kutengeneza taarifa na vipindi mbalimbali za redio, na hivyo kupata nafasi ya kuzungumzia kinachowagusa zaidi.

Ni namna gani redio imewawezesha katika maisha yao? Tuungane na watoto hao Tanzania, msimulizi wao ni Gertrude Clement kutoka Mwanza.