Mazungumzo ya Yemen Jumatatu, Ban apongeza

9 Februari 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekaribisha tangazo lililotolewa na mshauri wake maalum kuhusu Yemen, Jamal Benomar, ya kwamba Jumatatu ataitisha tena mashauriano ya kuleta maridhiano nchini humo.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Ban akipongeza vyama vyote vya siasa na majimbo nchini humo kuwajibika kama viongozi wa nchi hiyo ili kusongesha mbele Yemen wakati huu wa kipindi kigumu.

Mashauriano hayo yanawezeshwa na Umoja wa Mataifa ambapo Ban amesisitiza utayari wa chombo hicho kusaidia wananchi wa Yemen kufikia suluhu ya kisiasa kwenye mkwamo wa sasa.

Amesihi pande zote kuazimia kumaliza hali ya mpito wa kisiasa kwa mujibu wa mpango wa baraza la ushirikiano la nchi za ghuba na makubaliano ya mjadala wa kitaifa wa amani.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote kushauriana kwa nia njema wakiwa tayari kulegeza misimamo yao huku akiwakumbusha umuhimu wa kutoa ushirikiano kwa Benomar ambaye yeye Ban anamuunga mkono.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter