Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hafla yafanyika kuadhimisha wiki ya uwiano baina ya imani mbalimbali

Hafla yafanyika kuadhimisha wiki ya uwiano baina ya imani mbalimbali

Hafla maalum imefanyika leo kwenye Umoja wa Mataifa kuadhimisha wiki ya uwiano baina ya imani mbalimbali za kidini. Katika ujumbe wake, Rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa, amesema, kutokana na hali ilivyo duniani sasa, ujumbe wa amani na kutenda wema ni muhimu mno, hususan hali ya kutovumiliana na ubaguzi miongoni mwa jamii nyingi.

“Wakati kutovumiliana, udhalilishaji na chuki vinavyoendelea kuchochea migogoro, ukatili na misimamo mikali katika pembe nyingi za dunia, tunapaswa kuimarisha juhudi zetu za kuendeleza heshima na uelewano baina ya tamaduni, dini na makabila mbali mbali. Kila wakati tunapochagua mazungumzo na maridhiano badala ya vurugu, tunapiga hatua ya pamoja kwenye barabara ya amani ya kudumu.”

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa wiki hii inaadhimisha misingi ya kuvumiliana na heshima baina ya wanadamu, ambayo ni maadili yanayotokana na dini kuu duniani. Ban amesema maadhimisho haya pia ni wito wa kushikamana katika kukabiliana na wale wanaoeneza kutoelewana na kutoaminiana.

Ujumbe wa Ban umesomwa na Msaidizi wake na mkuu mpya wa Idara ya Habari na Mawasiliano kwenye Umoja wa Mataifa, Cristina Gallach.

"Jamii nyingi sana duniani zinakabiliwa na ukatili na ubaguzi kwa misingi ya dini zao. Waoga wanawashambulia raia. Wanasiasa wanatumia kauli za kuzua hisia ili kuwadangaya watu kwa misingi ya dini zao. Wanaoeneza machafuko na chuki wanatumia jina la dini, lakini wanapotosha tu mafunzo ya dini hizo na kujiaibisha.”

Ban amesema watu katika jamii na viongozi wa kidini wana ushawishi mkubwa mno, na wanaweza kuwa nguvu za ushirikiano, kujifunza, kufariji na maendeleo endelevu.