Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maziwa na mito ni muhimu kwa uhai wa mamilioni ya watu- FAO

Maziwa na mito ni muhimu kwa uhai wa mamilioni ya watu- FAO

Vyanzo vya samaki na maji safi ndani ya nchi kama vile maziwa na mito, na ambavyo hutegemewa na mamilioni ya watu duniani, vinapaswa kulindwa vyema zaidi ili kutunza mchango vinaoutoa kwa lishe na uchumi, hususan katika nchi zinazoendelea. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa Assumpta)

Hilo ni moja ya mapendekezo muhimu ya wataalam wa kimataifa kwenye kongamano la kimataifa kuhusu vyanzo vya samaki vya ndani ya nchi, ambalo limehitimishwa wiki hii mjini Roma, Italia.

Wakati wa kongamano hilo, watafiti mashuhuri katika sekta ya uvuvi na udhibiti wa maji, pamoja na makundi ya watu wa asili, walionya kuwa uhaba wa takwimu na sera mwafaka unachangia maamuzi yasiyozingatia vitu vinavyodhuru vyanzo vya samaki vya ndani ya nchi.

Devin Bertley ni afisa mwandamizi wa masuala ya samaki, FAO.

(Sauti ya Devin)

"Kote ulimwenguni hatujui ni kiasi gani kinavuliwa na nini,  ni aina gani inavuliwa. Uzalishaji halisi unaweza kuwa mara Tano zaidi ya ripoti zinazowasilishwa rasmi FAO. Na kuhusu aina ya samaki wanaovuliwa, wengi husema tu Samaki! Kwa hiyo hatufahamu aina ya samaki wanaovuliwa. Aidha tunajua mfumonuai wa maji ya mito na maziwa uko hatarini kwa samaki kupoteza maeneo yao, uchafuzi na uvuvi usio endelevu."

Maziwa na mito ni vyanzo vya protini, vitamin, mafuta na lishe hususan katika nchi zinazoendelea, ambako zaidi ya watu milioni 60 wanavitegemea kuishi.

Nchi zipatazo 71 zenye vipato vya chini huzalisha takriban tani milioni 7 za samaki, ambayo ni asilimia 80 ya samaki wanaovuliwa kote duniani, lakini maji wanamovuliwa samaki hao yanakabiliwa na shinikizo la mahitaji mengine ya binadamu kama vile uzalishaji nishati, utalii na kushindania maji safi.