Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na El Salvador kushirikiana kuimarisha amani

UM na El Salvador kushirikiana kuimarisha amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameshiriki maadhimisho ya miaka 23 ya makubaliano ya amani yaliyomaliza machafuko nchini  El Salvador ambapo amesema nchi hiyo ni mfano wa jinsi maridhiano yanavyoweza kurejesha maelewano.

Akizungumza katika hafla hiyo mjini San Salvador, Ban amesema El Salvador imedhihirisha kuwa hata baada ya vita vya zaidi ya muongo mmoja vilivyosababisha vifo vya watu zaidi ya Elfu 75, wananchi walikuwa jasiri na walitumia busara kumaliza tofauti zao na kujenga jamii inayoheshimiana na kuvumiliana.

Hivyo amesema mkataba uliorejesha amani umedhihirisha kuwa amani ni mchakato ambao unapaswa kujengwa na kuimarishwa kila siku ambapo akizungumza na waandishi wa habari amesema bado kuna changamoto nyingi za kushughulikia ikiwemo usalama na ghasia na machungu yanayokumba baadhi ya familia. 

Ban amesema anatambua kile wanachokabiliana nacho na kwamba..

“Ninatiwa moyo na kuundwa kwa baraza la taifa la usalama wa raia na uwepo wa pamoja. Umoja wa Mataifa uko tayari kuendelea kushiriki mchakato huu. Ninatiwa moyo kuwa Tume ya usalama ya Taifa imewasilisha mapendekezo yake jana kwa Rais na tumejadili na Rais na Umoja wa Mataifa uko tayari kuunga mkono mapendekezo hayo.”