Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio dhidi ya DPRK lapendekeza suala kuwasilishwa ICC

Picha ya UM/Maktaba

Azimio dhidi ya DPRK lapendekeza suala kuwasilishwa ICC

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK, likiamua pamoja na mambo mengine kuwasilisha mbele ya Baraza la Usalama ripoti ya Tume iliyochunguza ukiukwaji huo wa haki.

Azimio hilo ambalo lilipitishwa kwa kura 116, huku mataifa 20 yakipinga na mengine 53 kutoonyesha msimamo wowote, linataka Baraza la usalama lizingatie mapendekezo ya Tume na kuchukua hatua stahili za kuhakikisha uwajibikaji ikiwemo kuwasilisha suala hilo kwenye mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC.

 Halikadhalika Baraza kuu linataka baraza la usalama liangalie pia uwezekano wa vikwazo dhidi ya wakiukwaji wa haki kama ilivyobainishwa kwenye ripoti ya tume.

 Baadhi ya haki zilizobainishwa kukiukwa kwa mujibu wa azimio hilo ni pamoja na zile za kiuchumi, kijamii na kitamaduni ambazo zimesababisha njaa na tapiamlo hususan kwa watoto, wanawake, watu wenye ulemavu na wazee.