Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM wamuomba Obama kutoa ripoti ya CIA kuhusu kuhoji washukiwa

Rais Barack Obama wa Marekani akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. (Picha:UN/Mark Garten)

Wataalam wa UM wamuomba Obama kutoa ripoti ya CIA kuhusu kuhoji washukiwa

Kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu wametoa wito kwa Rais wa Marekani Barack Obama kusaidia kikamilifu uwezekano wa kutolewa kwa ripoti juu ya mpango wa kuhoji washukiwa wa Shirika la Kijasusi la Marekani, CIA iliyofanywa na Kamati Teule ya Seneti ya Marekani kuhusu upelelezi.

Katika barua ya wazi iliyotolewa jana, wataalamu hao walisema kuwa uamuzi wa Rais Obama kuhusu ripoti hiyo utafuatiliwa kwa karibu na waathirika wa utesaji na mataifa mengine na itakuwa na matokeo makubwa kwa waathirika wa ukiukwaji wa haki za binadamu kila mahali na pia imani kwa mfumo wa Marekani.

Wataalamu hao pia wamesihi, kama taifa ambalo hadharani linashikilia imani kwamba kuheshimiwa kwa ukweli kunapelekea kuheshimiwa kwa utawala wa kisheria, na kama taifa ambalo mara nyingi limetoa wito kwa mataifa mengine kuwa wazi na kuwajibika, basi Marekani itimize viwango ambavyo imejiwekea na wengine.

Uchunguzi huo wa Kamati ya Baraza la Seneti iliyozinduliwa mapema 2009, ulichukua miaka minne na kama sehemu ya uchunguzi wake ilikagua mamilioni ya kurasa za nyaraka ya shirika la CIA na barua pepe.