Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 370,000 hufariki dunia kila mwaka kwa maji –WHO

UN Photo/Tobin Jones)
Watu wakiogelea, Mogadishu, Somalia

Watu 370,000 hufariki dunia kila mwaka kwa maji –WHO

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni WHO imesema kuwa kwa wastani zaidi ya watu 370,000 hufariki dunia kila mwaka kwa maji wanapozama, huku ikitaja pia hatari inayowaandama watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Taarifa kamili na Joshua Mmali

(Taarifa ya Joshua)

Ripoti hiyo imebainisha maeneo ambayo matukio hayo yanajitokeza ni pamoja na katika sehemu za kuogea ambako watu bila kutarajia huzama na kupoteza maisha.

Katika ripoti yake hiyo WHO imesema kuwa matukio hayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika mito, kwenye visima vya kuogelea na hata kwenye matanki na mabeseni ya kuhifadhia maji.

 Dkt. Etienne Krug, ni Mkurugenzi wa WHO kuhusu udhibiti wa magonjwa yaso ya kuambukiza, ulemavu na kuzuia majeraha

“Kila saa, kila siku, zaidi ya watu 40 hufariki dunia kwa kuzama. Aghalabu watu hawa ni watoto katika mabeseni au katika visima vya maji na mito, wavuvi wanapofanya kazi yao ya kila siku majini, wahamiaji wanapotafuta maisha bora, lakini badala yake wakiyapoteza kwenye vivuko hatarishi, pamoja na feri zinazozama na kuwaua abiria wengi. Kwa ujumla, ni kuzama huchangia hadi vifo 372,000 kila mwaka”

Hata hivyo takwimu hizo hazijajumuisha matukio ya watu wanaofariki kwa mafuriko ama wale wanaochukua uamuzi wa kujiua.