Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO yapongeza makubaliano ya G20 yaliyofikiwa Australia

G20 Australia.(Picha ya ILO)

ILO yapongeza makubaliano ya G20 yaliyofikiwa Australia

Wakati mkutano wa kundi la nchi 20 zenye nguvu kubwa duniani ukimalizika huko Brisbane, Australia, Shirika la kazi duniani ILO limesema kuwa limetiwa moyo na ahadi zilizotolewa na viongozi ambao wamejizatiti kuongeza kiwango kipato na kukabiliana na changamoto za ajira duniani. Taarifa kamili na George Njogopa(Taarifa ya George)

Mkutano huo ambao uliangazia pia agenda nyingine za maendeleo umetaja mikakati ya kuongeza kwa asilimia mbili kiwango cha ukuaji uchumi wa dunia jambo ambalo litasaidia kwa sehemu kubwa kuboresha ustawi wa wananchi.

Akuzungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder amesema kuwa ni dhahiri kuwa makubaliano hayo yatakayofikiwa mwaka 2018 kuwa ni hatua kubwa ambayo yataleta mwanga wa matumaini mapya kwa mamia ya wananchi wanaohangaika kusaka fursa za ajira.

Alisema kuwa kutimia kwa agenda hiyo kutasaidia kwa sehemu kubwa kupunguza pengo la ajira baina ya nchi jambo ambalo kwa maoni yake itakuwa kama mwarobaini wa kufukia mabonde ya kimaendeleo yaliyosababishwa na mtikisiko wa kiuchumi ulioikumba dunia katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa upande mwingine mkuu huyo wa ILO aliopongeza tamko la pamoja lilitolewa na viongozi hao wa G20 kuhusiana na ugonjwa hatari wa ebola ambao umeziathiri zaidi nchi za Afrika magharibi.