Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa Maalum wa UM kuhusu Syria akutana na Rais Assad

Staffan de Mistura, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Syria. (Picha:UN/Mark Garten)

Mjumbe wa Maalum wa UM kuhusu Syria akutana na Rais Assad

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura, leo amekuwa na mazungumzo na mjini Damascus na Rais Bashar al-Assad na maafisa wa serikali yake kuhusu mapendekezo aliyowasilisha kwa Baraza la Usalama tarehe 30 Oktoba 2014.

Mapendekezo hayo yanahusu utekelezaji wa maazimio husika ikiwa ni pamoja na azimio 2170 na 2178 ya Baraza la Usalama.

Katika taarifa, Bw de Mistura amesema anatambua dhamira iliyoonyeshwa na mamlaka ya Syria ya kufanya kazi na Umoja wa Mataifa ya kutekeleza pendekezo lake la kusitisha mapigano taratibu kwa kuanzia na mji wa Aleppo.

Mpango huo utawezesha kuweka mazingira ya kupunguza ghasia kutoka maeneo tajwa na hatimaye kuwezesha kurejea kwa hali ya kawaida na mwisho kufanikisha mchakato wa kitaifa wa kisiasa.

De Mistura na timu yake sasa wananuia kuendelea haraka kufanya kazi juu ya usitishaji mapigano Aleppo, kupitia majadiliano zaidi na mamlaka ya Syria, na mashauriano zaidi na pande zote husika.