Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana vigori wana mchango mkubwa:UNICEF

Wasichana vigori wana mchango mkubwa:UNICEF

Ikiadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo imeenda sambamba na kutimia kwa maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanza kuazimishwa kwa siku hii,shirika la umoja wa mataifa linalohusika na watoto UNIECEF limesema kwamba wasichana vigori wanamsaada mkubwa kwa familia zao pamoja na jamii kwa ujumla.

UNICEF imesema kuwa zaidi ya wasichana vigori milioni 515 katika nchi zinazoendelea wameshika fungua wa kuzifanikisha jamii zao kupiga hatua kimaendeleo lakini kinachowakwamisha kukosekana kwa njia dhabiti ya kuwaendeleza kitaaluma na ujuzi wa maarifa.

Shirika hilo limeanisha kwamba mchango wa wasichana hao ni mkubwa na wenye uwezo wa kusukuma mbele maendeleo ya nchi zao lakini wanapaswa kufunguliwa milango kwenye maeneo ya elimu na kuungwa mkono kwa hali na mali.

Limesisitiza kwamba elimu ya sekondari kwa wasichana hao ni jambo lisilokwepeka kutokana na umuhimu wake ambao unawajengea mazingira ya kujiamini na hata kuwapa mwanga wa kukabiliana na changamoto mbalimbali kama manyanyaso ya kingono, kusafirishwa kwa njia haramu na kuzitetea haki zao za msingi.

Aidha limeongeza kuwa kuwapa elimu ya uhakika wasichana hao vigori ni kuwapa uwigo wa kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.