Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IMF yataja chanzo cha mkwamo bajeti ya 2014 Comoro

Nembo ya IMF

IMF yataja chanzo cha mkwamo bajeti ya 2014 Comoro

Shirika la fedha duniani, IMF limehitimisha ziara yake huko Comoro na kusema kiwango kidogo cha mapato na matumizi nje ya bajeti ndio chanzo cha mkwamo wa kiuchumi unaokumba nchi hiyo sasa licha ya kuwepo kwa maendeleo ya sera za uchumi mkuu.

Harry Trines kiongozi wa ujumbe huo amesema sera hizo zimesaidia mfumuko wa bei uliokuwa asilimia 3.5 mwishoni mwa mwaka jana kutarajiwa kupungua kwa angalau asilimia Sifuri nukta Saba mwishoni mwa mwaka huu na hata biashara ya nje kuongezeka

Hata hivyo IMF imesema licha ya nuru huyo bado utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2014 imekumbwa na mkwamo kwa kuwa fedha zilizopo hazijatosha kukidhi malipo ya mishahara ya walimu iliyoongezwa hivi karibuni na hata matumizi ambayo hayakuwa yamewekwa kwenye bajeti.

Trines amesema Comoro inatakiwa kutambua jinsi ya kupanga matumizi yake kulingana na rasilimali ilizo nazo ili kuepuka malimbikizo hususan kwenye mishahara ya wafanyakazi na ulipaji madeni.

Ameitaka Comoro iwekeze kwenye miundombinu, ichagize uchumi shirikishi na fursa za ajira.

Ziara hiyo ilifanyika kuanzia Oktoba 20 hadi tarehe Nne mwezi huu.