Athari za mabadiliko ya Tabianchi ni wazi, ni lazima tuchukue hatua za haraka: Ban

2 Novemba 2014

Ripoti ya tano ya Jopo la Kimataifa kuhusu Tabianchi , IPCC iliyotolewa Jumapili huko Copenhagen, Denmark imesema shughuli za binadamu zinazoathiri tabianchi zinazidi kuongezeka na athari zake kwa tabianchi ziko bayana kila bara.

Imetaka hatua za haraka zichukuliwe ikiwemo uamuzi mgumu wa kisiasa ili kuwepo na hatma endelevu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema ni wazi binadamu anazidi kusababisha madhara ya mabadiiko ya tabia nchi na iwapo dunia inataka kuepukana na madhara makubwa ni lazima hatua za haraka  zichukuliwe.
Amenukuu ripoti hiyo inayoeleza kuwa uwezo wa kudhibiti upo lakini bado dunia haijajiandaa vya kutosha kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi hususan maskini ambao nafasi yao katika mabadiliko hayo ni kidogo.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa IPCC RK Pachauri amesema njia za kudhibiti zipo lakini kinachotakiwa ni mabadiliko ya fikra katika kutambua uelewa wa sayansi ya mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti hiyo ya imeandaliwa na zaidi ya wanasayansi 800 katika kipindi cha miezi 13, hii ikiwa ni tathmini ya kina zaidi kuwahi kufanywa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na ina nafasi kubwa katika makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa mwakani huko Paris.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud