Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziara ya Ban Ushahidi/Ihub jijini Nairobi yamfungua mengi

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon (aliyesimama katikati) akizungumza na vijana baada ya kutembelea ofisi za Ushahidi/IHub jijini Nairobi. (Picha:Eskinder Debebe)

Ziara ya Ban Ushahidi/Ihub jijini Nairobi yamfungua mengi

Wakati akihitimisha ziara yake ya Pembe ya  Afrika huko Nairobi Kenya siku ya Ijumaa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon ametembelea ofisi ya Ushahidi/Ihub, ambayo ni ya shirika linalotumia teknolojia katika kukabiliana na changamoto za kisasa.

Ban amesema alitaka kuzuru ofisi hiyo ili kushuhudia mwenyewe mustakhbali wa Kenya, mustakbali wa wanawake na ule wa Afrika kwa ujumla.

Akizungumza kituoni hapo amesema ziara yake imemwezeha kushuhudia ubunifu unaoendelea kumpatia msisimko kwani hakuwa na ufahamu kuhusu baadhi ya vitu vinavyotekelezwa kwenye kituo hicho .

Ametolea mfano wa teknolojia ya kuhamisha pesa kwa simu nchini Kenya, MPesa ambayo amesema zaidi ya asilimia 70 ya malipo hupitia huduma hiyo inayotumia mfumo wa teknolojia ya BRCK.

Ziara ya Ban kwenye kituo cha Ushahidi/Ihub ilinukuliwa pia na msemaji wake Stéphane Dujarric alipozungumza na waandishi wa habari.

(Sauti ya Dujarric)

"Katibu mkuu alitembelea ofisi za ushahidi/ Ihub zilizoko Nairobi ambacho ni kama tanuru la kuandaa vijana wa Kenya wabunifu. Alipongeza ubunifu wao na kubainisha mawazo yao yamesambazwa duniani.”

Aidha, Katibu Mkuu amesema amefurahia kuona vijana wengi wanawake  wanaotumia uwezo wa raslimali yao ya hali ya juu.