Taka za plastiki baharini zaharibu mikoko duniani

29 Septemba 2014

Uharibifu wa baharini, hasa kupitia taka za plastiki, huathiri kuwepo kwa mikoko na hugharimu zaidi ya dola bilioni 13 kila mwaka, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira, UNEP. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Ripoti iliyotolewa leo mbele ya mkutano mkuu wa viongozi na wanasayansi kuhusu utunzaji wa bahari imeonyesha kuwa mikoko huharibika duniani kwa kasi kubwa, mara tano zaidi ya uharibifu wa misitu.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya jumatatu tarehe 29 Septemba, mkurugenzi mkuu wa UNEP, Achim Steiner, amesema robo ya mikoko iliyopo duniani imeshapotea, kutokana na uchafuzi wa mazingira, kuwepo kwa taka za plastiki baharini, ufugaji wa samaki, kilimo, na mabadiliko ya tabianchi.

Ameomba hatua zichukuliwe haraka ili kusitisha uharibifu huo, kwani zaidi ya watu milioni 100 hutegemea mikoko kuishi, hasa kwenye nchi zinazoendelea. Juu ya hayo, ameeleza, mikoko huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuzuia kuwepo kwa hewa ya ukaa angani.

Utunzaji wa mikoko pamoja na mikakati mingine ya kutunza bahari, vinaangaziwa katika mkutano wa 16 wa mikataba ya bahari unaofanyika mjini Athens, Ugiriki.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter