Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awambia viongozi wa dunia hatuko hapa kuongea bali kuleta mabadiliko

UN Photo/Amanda Voisard
UN Photo/Amanda Voisard

Ban awambia viongozi wa dunia hatuko hapa kuongea bali kuleta mabadiliko

Leo siku ya tarehe 23 Septemba, zaidi ya viongozi 120 wa dunia pamoja na wawakilishi wa jamii na mashirika yasiyo ya kiserikali wanakutana katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kwa ajili ya kongamano kubwa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza katika uzinduzi wa mkutano huo, baada ya kuangalia filamu ya kuelimisha watu kuhusu athari na fursa zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema mabadiliko ya tabianchi yanaweka hatarini usalama, maendeleo na ndoto za watu duniani kote:

“ Hatujawahi kukabiliana na tatizo kama hili. Na hatujawahi kupata fursa kubwa kama hii. Maisha ya baadaye yatakayoweza kukabiliana na tabianchi, yenye kaboni kidogo yatakuwa maisha bora, yenye usafi, afya, usawa na utulivu zaidi si kwa wachache lakini kwa kila mtu.”

Katibu Mkuu ameongeza kuwa kuna kizuizi kimoja tu, ambacho ni sisi binadamu. Amesema ndiyo maana amewaomba viongozi wote wa dunia wawajibike na waongoze katika kuleta mabadiliko, ili kupunguza kwa nyuzi mbili halijoto ya dunia.

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Sam Kutesa, amesisitiza malengo ya mkutano huo:

“Tunakusanyika hapa na dhamira mbili: kuchagiza utashi wa kisiasa ili kukamilisha mkataba yakinifu wa mabadiliko ya tabianchi mjini Paris Disemba 2015, na kuibua hatua mathubuti za kuongeza uhimili na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kuuelekeza ulimwengu kwenye uchumi unaojali mazingira.”

Kwa upande wake, meya wa New York Bill de Blasio amesema halmashauri ya jiji kuu la New York limeamua kujituma:

"Jumapili nimetangaza kwamba mji wa New York unajituma kupunguza gesi chafuzi kwa asilimia 80 ifikapo 2050. Sisi ndio mji mkubwa zaidi duniani kuamua kutekeleza mpango mathubuti kama huo".