Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya dola bilioni 200 zaahidiwa kufadhili upunguzaji wa kaboni na uhimili wa tabianchi

UN Photo/Rick Bajornas)
Katibu mkuu Ban akihutubia mkutano wa tabianchi wa 2014. Picha:

Zaidi ya dola bilioni 200 zaahidiwa kufadhili upunguzaji wa kaboni na uhimili wa tabianchi

Viongozi wa serikali, jamii ya wawekezaji na taasisi za fedha wametangaza leo kuchagiza mamia ya mabilioni ya dola ili kufadhili upunguzaji wa hewa ya mkaa na kuweka njia za kuhimili tabianchi.

Ahadi hizo zinalenga kupata zaidi ya dola bilioni 200 za fedha, na hivyo kupanua fursa za uwekezaji wenye faida za kijamii na kuimarisha uhimili wa tabianchi kote duniani, ikiwemo katika nchi zinazoendelea na nchi za visiwa vidogo zinazoendelea.

Tangazo hilo linajumuisha mseto wa ufadhili wa umma na kibinafsi, pamoja na ahadi za wahisani na nchi zinazoendelea ili kuupanua mfuko wa tabianchi endelevu.

Fedha hizo zinatarajiwa kuwepo ifikapo mwisho wa mwaka 2015, wakati serikali zikihitimisha mkataba mpya wa kimataifa kuhusu tabianchi.

Ahadi hizo mpya zitatoa msukumo mkubwa kwa juhudi za kuchagiza dola bilioni 100 kila mwaka ifikapo mwaka 2020, ambazo ziliahidiwa kwa ajili ya ufadhili wa tabianchi katika nchi zinazoendelea. Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameelezea hisia zake kufuatia hatua hiyo ya leo.

“Nimefurahia mno ufadhili ambao umechagizwa kwenye mkutano huu na sekta za umma na binafsi. Hili litatia chachu katika kukamilisha mktaba jumuishi na yakinifu mjini Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi mwaka 2015. Mkutano huu umeweka jukwaa la ushirika mpya na kuwafanya viongozi kutoka sekta za umma na binafsi kote duniani kutambua sio tu hatari za tabianchi, bali pia kukubaliana kufanya kazi pamoja.”