Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu anaweza kuchangia katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi

UN Photo/Marco Dormino
Walinda amani wa MINUSTAH wakisaidia wahanga wa mafuriko nchini Haiti. @

Kila mtu anaweza kuchangia katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Viongozi wa dunia wakikutana leo tarehe 23 Septemba kwa ajili ya kujadili mabadiliko ya tabianchi,  Cassie Flynn, ambaye ni mtalaam wa mabadiliko ya tabianchi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP amesema kuna changamoto mbili muhimu zinapaswa kukabiliwa.

Ya kwanza ni utoaji wa gesi chafuzi unaosababisha kwa kiasi kikubwa katika mabadiliko ya tabianchi, Bi. Flynn akisema kwamba ni muhimu kujitahidi kuupunguza.

Changamoto ya pili, kwa mujibu wake, ni kujiandaa na kujitayarisha ili kuweza kukabiliana na matokeo ya mabadiliko ya tabianchi yakiwemo hatari za mafuriko makubwa. Amesema ni lazima jamii na serikali waandae mifumo ya tahadhari ili kupambana na hatari hizo.

Halikadhalika mtalaam huyo amesisitiza hali ya nchi za visiwa vidogo ambazo zimejitahidi kubaini njia mbadala za kukumbana na athari za mabadiliko ya tabianchi wakati nchi hizo hazina njia yoyote ya kuepuka na matokeo ya ongezeko la maji baharini.

Hatimaye ametaja mifano ya hatua rahisi zinazoweza kuchukuliwa kukabiliana mabadiliko ya tabianchi:

“ Kuna vitu vingi raia wa kawaida wanaweza kufanya ili kuleta mabadiliko. Mfano wa kwanza ni kujali matumizi yako ya nyumbani. Kwa mfano ukienda dukani kununua balbu ya umeme., labda utakuta aina mbili za balbu: zinazotumia nishati nyingi na zinazotumia nishati kidogo. Ukianza kununua balbu za umeme zinazotumia nishati kidogo, unafanya kitu cha kuonekana kinachochangia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi”