Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame na mabadiliko ya tabianchi vinaathiri ukanda wa nchi za Kiarabu

Mradi wa pamoja wa kumaliza gesi chafuzi ya carbon nchini Iran.© Pasha Tabrizian

Ukame na mabadiliko ya tabianchi vinaathiri ukanda wa nchi za Kiarabu

Ukame wa kilimo na mabadiliko ya tabianchi vinabadilisha hali katika ukanda wa nchi za Kiarabu na kuwa na athari kubwa mno kwa usalama wa chakula, uhamiaji mijini na ustawi wa kijamii, amesema mtaalam anayeshauri Umoja wa Nchi za Kiarabu wakati wa kongamano la pili la muungano huo kuhusu kupunguza hatari za majanga.

Profesa Wadid Erian amesema kuwa kulikuwa na upungufu wa asilimia 12.6 ya uzalishaji wa kilimo katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, ukisababishwa na ukame ambao pia umechangia kupoteza eneo kubwa la ardhi inayoweza kulimwa.

Ametoa mfano wa ekari milioni 200 za ardhi kwenye eneo zima ambalo limeathiriwa na ukame na mmomonyoko wa udongo, ambavyo vinasababisha watu kuhama na kuongeza hatari ya kuwepo mizozo. Ameongeza kuwa zaidi ya ekari milioni 60 za ardhi kwenye eneo hilo zimeharibiwa kwa kiasi kisichoweza kurekebishwa. Nchi zilizoathiriwa zaidi ni Djibouti na Palestina.

Mtaalam huyo ametoa wito mkakati wa kupunguza hatari za majanga ujumuishwe katika ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, ili kujali hatma ya watu bilioni 2 duniani wanaoishi katika maeneo yenye ukame, ambayo ni asilimia 41 ya ulimwengu mzima.