Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iraq inakabiliwa na tatizo sugu la kibinadamu- Mkuu wa OCHA

Mkuu wa OCHA, Bi. Valerie Amos (Picha ya UM)

Iraq inakabiliwa na tatizo sugu la kibinadamu- Mkuu wa OCHA

Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura, Valerie Amos, amesema leo kuwa nchi ya Iraq inakabiliwa na tatizo sugu la kibinadamu, huku watu wapatao milioni 1.8 wakiwa wamelazimika kuhama makwao tangu mwezi Januari mwaka huu, wengi wao wakiishi na jamaa zao na wengine katika manjengo yaliyoachwa.

Mkuu huyo wa OCHA amesema watu milioni 20 kote nchini Iraq wameathiriwa tangu wimbi la kwanza la wakimbizi liliposhuhudiwa mnamo mwezi Januari, na kuongeza kuwa wakati huu msimu wa baridi unapokaribia, kuna kazi nyingi ya kufanya ili kuhakikisha kuwa familia hizo za wakimbizi wa ndani zinalindwa kutokana na baridi kali.

Bi Amos amesema hayo baada ya kuizuru kambi ya Khanke, Dohuk, ambayo ndiyo kubwa zaidi nchini humo. Amesema familia za wakimbizi aliozungumza nao wanasema  wameshuhudia ukatili mbaya mno dhidi ya watoto, wanawake na wanaume kutoka kwa kundi la ‘Da’ash’, na kile wanachotaka wengi wao ni kurejea makwao tu.