Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu asihi Urusi na Ukraine kuzuia kudorora uhusiano kati yao

Mkazi wa eneo la Artema ambalo ni moja ya viunga vya mji wa Sloviansk, nchini Ukraine, akiwa katika mabaki ya eneo ambalo awali lilikuwa jiko wakati wa msimu wa kiangazi. (Picha:UNHCR/Iva Zimova)

Katibu Mkuu asihi Urusi na Ukraine kuzuia kudorora uhusiano kati yao

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa ripoti kwamba msafara wa magari yenye misaada kutoka Urusi imevuka mpaka na kuingia nchini Ukraine bila ya idhini ya serikali Ukraine.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa katika taarifa amemkariri Ban akisema kuwa pamoja na kutambua kudorora kwa hali ya kibinadamu, hatua ya upande mmoja ya kufanya uamuzi bila mashauriano inaweza kusababisha kuharibika kwa hali ambayo tayari ni mbovu Mashariki mwa Ukraine.

Kwa mara nyingine Katibu Mkuu ameagiza pande zote hususan Ukraine na Urusi kuendelea kufanya kazi pamoja wakishirikiana na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa misaada ya kibinadamu inawafikia wanaohitaji zaidi.

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu amesema ametiwa moyo na na tangazo la Rais wa Ukraine Petro Poroshenko kuwa watafanya kila wawezalo kuzuia athari zaidi kufuatia msafara wa magari ya misaada ya Urusi kuingia nchini Ukraine.