Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua nne zahitajika kuhimiza malengo ya milenia

UN photos/ Mark Garten
@

Hatua nne zahitajika kuhimiza malengo ya milenia

Leo ikiwa imebaki siku 500 tu kabla ya kufikia ukomo wa malengo ya maendeleo ya milenia yaliyoamuliwa na viongozi vya dunia, mwaka 2000, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mtaifa Ban Ki-Moon ametuma ujumbe wake ili kuongeza jitihada za kuhimiza malengo hayo.

Amesema, ingawa dunia imepitia matatizo megi tangu 2000, yakiwemo vita, mzozo wa kiuchumi, majanga ya hali ya hewa, mafanikio yapo ikiwemo umaskini kupunguzwa kwa asilimia hamsini, wasichana zaidi wapo shuleni, wanawake wengi zaidi wanajifungua bila shida na familia nyingi zaidi zinapata maji safi na salama.

Hata hivyo Ban katika taarifa yake amesema bado jitihada zinahitajika, akitaja hatua nne zinazofaa kuchukuliwa ili kuongeza kasi ya utekelezaji.

Mosi, ni kuwekeza pesa katika sekta ya afya, elimu, nishati na maji safi, kwa kuwezesha wasichana na wanawake.

Pili, kulenga nchi maskini zaidi na jamii zilizo kwenye mazingira magumu zaidi, ambazo zina kazi kubwa zaidi licha ya jitihada zao, tatu, ni kuheshimu ahadi za ufadhili,

Hatua ya Nne kwa mujibu wa Ban ni kuimarisha ushirikiano baina serikali, jamii, sekta binafsi na mitandao mbali mbali duniani, akisema kwamba changamoto ni nyingi, lakini mbinu zipo nyingi kuliko ilivyokuwa mwanzo wa karne ya 21 kuanzia uwezo wa kiteknolojia hadi ongezeko la uelewa wa kile kinachofaa na kisichofaa.