Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku 500 kabla ya ukomo wa maendeleo, tuchukue hatua:Ban

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon na Malala Yousfzai katika mjadala huo. (Picha:UN/Mark Garten)

Siku 500 kabla ya ukomo wa maendeleo, tuchukue hatua:Ban

Ikiwa zimebakia siku 500 kabla ya kufikia ukomo wa malengo ya maendeleo ya milenia, katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa Ban Ki-Moon amezungumza kwenye tukio maalum mjini New York akichagiza ufikiaji wa malengo hayo. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

(Taarifa ya Grace)

Tukio hilo lilihusisha mjadala kati ya Katibu mkuu Ban na Mwanaharakati wa kike aliyenusurika kifo hukoPakistan, Malala Yousfzai, ukijikita katika kasi inayopaswa kuchukuliwa ikiwa ni siku 500 kabla ya ukomo wa malengo ya maendeleo ya milenia.

Ban katika utangulizi wake akasema duniani bado kuna mizozo ya kisiasa, umwagaji damu, dharura za afya ya umma na ukiukwaji wa haki za binadamu!

Amesema safari ilikuwa ndefu ingawa hali si shwari, bado kuna matumaini akitaka vijana ambao wana nafasi kubwa kujifunza kutoka kile alichofanya akiwa mtoto na kijana huko Korea baada ya vita!

(Sauti ya  Ban)

"Unavyojua, nimelelewa kwenye nchi iliyoathiriwa na vita, Korea. Wakati huo, kila kitu kilikuwa kimeharibika. Hatukuwa na madarasa, tulisoma chini ya mti. Lakini tulikuwa na kiu ya kupata elimu. Ndiyo maana niko hapa. Ndiyo maana nawaambia watoto wote ambao wanakumbwa na changamoto ya kupata elimu, msikatae tamaa!" 

Malala akasema ziara zake duniani kote baada ya ajali iliyompata imemfundisha mambo mengi kuwa elimu inaweza kubadilisha dunia na hata kufikia malengo  ya milenia akitoa mfano..

(Sauti ya Malala)

"Zamani walikuwa wanafikiria mtu anayeua zaidi ya simba mmoja ndiye shujaa wa kimaasai. Sasa wamebadilisha mawazo, mtu yeyote, msichana au mvulana ambaye anamaliza masomo yake, ambaye anapata cheo cha juu cha elimu ndiye anakuwa shujaa wa kimaasai. Wamebadilisha kabisa maoni yao kuhusu ushujaa."