Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola ni dharura ya afya ya umma duniani; hakuna zuio la safari au biashara:WHO

Mwanamke asubiri kuingia kumlisha mumewe katika wadi iliyotengwa inayofadhiliwa kwa pamoja na wizara ya Liberia, WHO na MSF wanaotoa huduma kwa wagonjwa katika mji mkuu Monrovia.Picha UNMIL/Staton Winter

Ebola ni dharura ya afya ya umma duniani; hakuna zuio la safari au biashara:WHO

Hatimaye shirika la afya duniani WHO limetangaza ugonjwa wa Ebola kuwa ni dharura ya afya ya umma duniani wakati huu ambapo umeshasababisha vifo vya watu zaidi ya 900 huko Afrika Magharibi huku likieleza bayana hakuna zuio la biashara au safari kutokana na mlipuko huo. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

WHO imesema mlipuko wa Ebola unahatarisha afya ya  umma kwenye mataifa mengine na imetaka mshikamano wa kimataifa kusaidia nchi zilizokumbwa na ugonjwa huo kuweza kukabiliana nao.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan amesema kuenea kwake hukoLiberia,Sierra Leone na Guinea kumechochewa na mfumo wa afya ulioporomoka, uhaba wa vifaa tiba na wahudumu wa afya waliobobea pamoja na fikra potofu za umma juu ya ugonjwa huo.

(Sauti ya Dkt. Chan)

Kutangaza Ebola ni hofu ya kimataifa kwa afya ya umma inatoa tahadhari kwa dunia juu ya umuhimu wa kuwa macho kwa uwezekano wa kubuka visa zaidi. Lakini haimaanishi kuwa nchi zote au hata nchi nyingi zaidi zitashuhudia visa vya Ebola. Hizi nchi ndio kwanza zimetokea kwenye miongo ya vita na magumu. Kwa hiyo iwapo hatutazisaidia, zitarudishwa nyuma miaka mingi zaidi.”

Ilikudhibiti kuenea zaidi duniani, WHO imesema wasafiri wote kutoka nchi zilizokumbwa na ugonjwa huo wanapaswa kuchunguzwa iwapo wana dalili za Ebola na wale tayari walioambukizwa hawapaswi kuhamishiwa nchi nyingine.

Naye Mauricio Ferri ni daktari kutokaBrazil ambaye alitumwa kwenda Sierra Leone kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola mara baada ya mlipuko anasema kila siku walipokea wagonjwa wapatao 50 na angalau 30 walithibitika kuwa na Ebola huku mazingira ya utabibu yakiwa magumu.

(Sauti Dkt. Ferri)