Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani mauaji ya wafanyakazi wa kibinadamu Sudan Kusini

Kikao cha baraza la usalama.Picha/UM/NICA

Baraza la Usalama lalaani mauaji ya wafanyakazi wa kibinadamu Sudan Kusini

Baraza la Usalama limelaani vikali mashambulizi yaliyotokea hivi karibuni dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu huko Sudan Kusini wakati wanamgambo wajiitao  Jeshi la Ulinzi  wa Maban walipokabiliana na askari wa jeshi la kitaifa SPLA  wenye asili ya Nuer.

Rais wa Baraza la usalama Balozi Mark Lyall Grant amesema wajumbe wamesema mauaji hayo yanaweza kuwa uhalifu wa kivita wakisema..

(Sauti ya Balozi Grant)

“Tumekubali sote kwamba tumesikitishwa na hali ya Sudan Kusini, kuendelea kwa mapigano na kushindwa kupata sukuhu katika mazungumzo ya amani. Tunaunga mkono uongozi wa IGAD katika mazungumzo hayo. Kila mtu amehisi kwamba ziara ya Baraza la Usalama nchini humo inakuja muda mwafaka, na itakuwa fursa ya kutuma ujumbe mzito kwa viongozi wawili kuhusu umuhimu ya kushirikiana vizuri katika mazungumzo ya IGAD.”

Hatimaye, walitoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini ihakikishe hali ya usalama kwa raia wake na ipeleke watekelezaji wa mauaji hayo mbele ya sheria.