Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awakutanisha wawakilishi wapya kuhusu Syria na wanahabari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akutana na Staffan de Mistura(kushoto) na Ramzy Ezzeldin Ramzy katika makao makuu(Picha/UM/Eskinder Debebe/NICA)

Ban awakutanisha wawakilishi wapya kuhusu Syria na wanahabari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, leo amemtambulisha Mwakilishi wake mpya kuhusu Syria, Staffan de Mistura na makamu wake Ramzy Ezzeldin Ramzy kwa waandishi wa habari.

Akiwatambulisha wawili hao mjini New York, Bwana Ban ameelezea kubahatika kuweza kuwa na imani na hekima ya wanadiplomasia hao, ambao amesema watasafiri kwenda Syria, nchi za ukanda na nchi nyinginezo husika katika siku chache zijazo.

Bwana Ban amesema kuwa amewahakikishia wanadiplomasia hao ya kwamba atashirikiana nao kwa karibu sana kupitia ofisi zake na washauri wake wa ngazi za juu. Amesema kwa pamoja, watafanya juhudi zote ili kukomesha machafuko, na kufikia suluhu jumuishi la kisiasa linaloongozwa na watu wa Syria, na linalotimiza ndoto zao za demokrasia.

Uungwaji mkono kikamilifu wa pande zote na jamii ya kimataifa, hususan ukiwemo ule wa Baraza la Usalama, utakuwa muhimu. Watu wa Syria wamepitia machungu ya kutosha, na kwa muda mrefu sana. Ni wakati wa kuchukua hatua, na ni wakati wa amani.”

Wakati huo huo, Ban amezungumzia vitendo vya Israel kuanza mashambulizi ya ardhini dhidi ya Gaza, na kuelezea kusikitishwa na kwamba, licha ya wito wake wa mara kwa mara, mzozo huo hatari tayari umezidi kuwa mbaya hata zaidi.

Katika saa 24 zilizopita, kumekuwa na matukio kadhaa yaliyohusisha raia kuuawa, yakiwemo mauaji ya wavulana wanne ufukoni mjini Gaza. Natoa wito kwa Israel kujitahidi zaidi kukomesha vifo vya raia. Hakuwezi kuwa na suluhu la kivita kwa mzozo huu. Hili linahusu mzozo wa Israel na Palestina, na vile vile wa Syria.”

Ban pia amezungumza kuhusu baa la ndege ya Malaysia, akisema kuwa anafuatilia kwa karibu ripoti, zikiwemo zile za Shirika la Kimataifa la Safari za Angani. Amesema ni dhahiri kuwa kuna haja ya uchunguzi wa kimataifa wa kina na wazi, na kutuma rambi rambi zake kwa familia za wahanga na watu wa Malaysia.